TAEC YAONESHA MCHANGO WA TEKNOLOJIA YA NYUKLIA KATIKA AFYA NA KILIMO




Na Mwandishi Wetu - Dodoma


Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imehitimisha kwa mafanikio ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambapo ilitoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya mionzi na mchango wa teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Katika kipindi chote cha maonesho hayo, banda la TAEC lilitembelewa na wananchi, wanafunzi, wataalamu na wadau mbalimbali waliopata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu ya Tume katika kusimamia matumizi ya mionzi nchini pamoja na kuhakikisha teknolojia ya nyuklia inatumika kwa kuzingatia viwango vya usalama vinavyolinda afya za binadamu na mazingira.

Wataalamu wa TAEC walitoa elimu kuhusu usimamizi na udhibiti wa matumizi ya vyanzo vya mionzi, utoaji wa vibali kwa watumiaji wa teknolojia hiyo pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara unaofanyika katika taasisi na maeneo mbalimbali yanayotumia vifaa vya mionzi ili kuhakikisha usalama unaendelea kuzingatiwa wakati wote.

Aidha, wananchi walipata uelewa kuhusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo, viwanda, migodi, maji na utafiti wa kisayansi. Elimu hiyo ilibainisha mchango mkubwa wa teknolojia hiyo katika kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa, kuongeza uzalishaji katika sekta za uzalishaji na kusaidia matumizi endelevu ya rasilimali za taifa.

Vilevile, TAEC ilitoa ufafanuzi kuhusu nafasi ya teknolojia ya nyuklia katika uzalishaji wa nishati ya umeme, ikieleza namna teknolojia hiyo inavyoweza kuchangia upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya kuendeleza shughuli za viwanda, biashara na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Katika sekta ya afya, wananchi walielimishwa kuhusu matumizi ya mionzi katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali, huku katika sekta ya chakula wakipata maelezo kuhusu matumizi ya teknolojia ya mionzi katika uhifadhi wa mazao na bidhaa za chakula kwa kuzuia uharibifu unaosababishwa na wadudu na vimelea, hivyo kuongeza muda wa matumizi na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Mbali na kupata elimu, washiriki wa maonesho hayo walipata fursa ya kuuliza maswali na kufanya majadiliano ya moja kwa moja na wataalamu wa TAEC kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa mionzi, hatua za tahadhari zinazopaswa kuzingatiwa pamoja na mchango wa Tume katika kulinda jamii dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama ya mionzi.

TAEC imeeleza kuwa ushiriki wake katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi, kutoa taarifa sahihi kuhusu huduma zake na kuongeza uelewa wa umma kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyohitimishwa leo yameendelea kutoa fursa kwa taasisi za umma kuwasilisha huduma zao kwa wananchi, kuimarisha uwajibikaji, kujenga imani ya umma na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wa taasisi hizo katika maendeleo ya Tanzania.











Post a Comment

0 Comments